Jumatatu, 25 Agosti 2014

Rasimu ya Katiba inataja Tunu za Taifa: Ni nani kati yetu anayezijua!

Ndesyu Florian


KWA UFUPI

Ni dhahiri, ndiyo maana hata wakati wa kuandika au kutunga kanuni zinazosimamia Bunge hilo, wengi walipinga kwa mfano uamuzi wa mambo kufanyika kwa njia ya kura ya wazi,waking’ang’ania usiri, ambao hakuna shaka ndiyo unaozaa maovu ambayo baadhi ya wanaCCM wakiwamo viongozi wanatuhumiwa nao.
Nimeamua leo nianze kwa kueleza kitu kinachoitwa tunu. Tunaambiwa na wataalamu wa Kiswahili kuwa tunu ni kitu anachopewa mtu na mwingine kuwa niishara ya mapenzi, hidaya, zawadi, adia, hiba, azizi.
Tafsiri nyingine ya Kiswahili ya tunu inaeleza kuwa ni kitu ambacho ni adimu kupatikana na chenye kutumika kwa nadra.
Nimetumia maneno tunu baada ya kusoma rasimu ya pili ya Katiba na randama yake na kukutana na neno hili ‘Tunu za Taifa’.
Nimebaini kumbe kuwa Tunu za Taifa ni baadhi ya mambo ambayo yalijadiliwa siku nyingi, yalishapita baada ya kuwa yamejadiliwa na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kule Dodoma, lakini bila kufikia mwafaka.
Kumbe, nimebaini kuwa mgawanyiko ndani ya Bunge hili ambalo mara zote nimesema kuwa limegawanyika na kubakia vipande, mgawanyiko wake ulianzia hapo.
Hivyo, nimeamua nikumegee msomaji leo japo kidogo kile kilichoandikwa ndani ya rasimu, kuhusu tunu hizi za Taifa, kitu ambacho huenda wapo baadhi yenu ambao hamjawahi kukiona au hata kukisoma.
Kifungu hiki kinatoka Sura ya Kwanza ya Rasimu, Ibara ya 5: Tunu za Taifa. Sehemu A- inazungumzia Maudhui ya Ibara. Kifungu hiki kinasomeka:
Ibara hii ya Rasimu ya Katiba inapendekeza kuwa Utu, Uzalendo, Uadilifu, Umoja, Uwazi, Uwajibikaji na Lugha ya Kiswahili ambayo ni lugha rasmi ya Taifa, ziwekwe katika Katiba kuwa ndizo Tunu za Taifa.
Binafsi, sina ubishi wowote kuhusu azma nzuri ambayo Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya Jaji Joseph Warioba iliiona wakati ule wa kuandika mambo haya ambayo yameandikwa na kuitwa Tunu za Taifa kwamba yana manufaa.
Haya ndiyo yameandikwa kwenye rasimu ya pili na ambayo inajadiliwa kwa sasa ndani ya Bunge hili ambalo hakuna shaka limemeguka na kubakia vipande, halina tena mshikamano, sifa kuu ambayo imewatambulisha na kuwabeba kwa miaka mingi Watanzania.
Nimesikia kutoka kwa baadhi ya watu waliokuwamo ndani ya Bunge hilo kuwa wakati wa kujadili sura hii ya kwanza ya rasimu, ambako nimeambiwa kuwa wajumbe waligawanyika kwa kiasi kikubwa.
Kwa bahati nzuri, wakati ule, wajumbe wale wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walikuwa bado ndani ya kikao hiki, nimeambiwa kuwa suala la Tunu za Taifa liliwachanganya wengi, kisha likawagawa. Kwa ufupi, hawakukubaliana.

Kamati za bunge maalumu la katiba, zimeendelea kupitia rasimu ya katiba.

Kamati za bunge maalumu la katiba, zimeendelea kupitia rasimu ya katiba huku baadhi zikiondoa vifungu ikiwemo kinachotakiwa mbunge kuongoza kwa mihula mitatu pekee na kile kinachowapa wananchi mamlaka ya kumuondoa mbunge pale wanapoona hafanyi kazi yake vizuri.
Mwenyekiti wa kamati namba tano, Mh Hamad Rashid amesema rasimu ni nzuri lakini kuna licha ya kuwa rasimu hiyo ilikuwa nzuri, ina baadhi ya mapungufu huku akigusia suala la mfumo wa muungano wa serikali tatu uliotaka bajeti ya jeshi igharamikiwe na nchi wahisani jambo alilosema endapo wananchi wa sehemu moja ya muungano wakilikataa, litasababisha jeshi kufanya mapinduzi na kuleta machafuko.
Kwa upande wake katibu wa bunge maalumu la katiba la katiba, Yahaya Hamad Hamissi, amesema kamati ya uongozi ya bunge hilo imeunda kamati ndogo ya watu 10 ili kushughulikia suala la mahakama ya kadhi na uraia pacha kutokana na vipengele hivyo kuwasumbua sana wajumbe.
Wakati baadhi ya wajumbe wa bunge hilo, taasisi mbalimbali pamoja na baadhi ya wanasiasa wakishauri kuahirishwa kwa bunge hilo hadi baada ya uchaguzi mkuu, baadhi ya wajumbe wameeleza wasiwasi wao juu ufinyu wa muda kwa madai kuwa wanajadilin kwa kulipualipua hali ambayo inaweza kuwafanya wasipate katiba bora.

Arfi naye kwenda kortini kupinga Bunge la Katiba

Dodoma. Mjumbe wa Bunge Maalumu, Said Arfi amesema anakusudia kwenda mahakamani kupata ufafanuzi wa uhalali wa Bunge hilo kuachana na Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na badala yake kufanya kile alichokiita kuandika rasimu nyingine.
Katika taarifa yake jana, Arfi alisema hatua yake ya kwenda mahakamani inatokana na ukweli kwamba baada ya Bunge Maalumu kukataa muundo wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, haiwezekani tena kujadili Rasimu ya Tume.
“Badala yake kinachofanyika kwa sasa ni kuandika rasimu nyingine ili iendane na muundo wa serikali mbili ambao ndiyo Chama cha Mapinduzi wanaoutaka,” alisema na kuongeza kuwa kinachofanyika sasa katika kamati ni mabadiliko makubwa ya Katiba ya sasa na siyo uandishi wa Katiba Mpya.
“Kimsingi, baada ya wabunge wanaotokana na vyama vinavyounda Ukawa kuondoka, ni kama sasa nyani amekabidhiwa shamba la mahindi lisilo na mlinzi. Kwa hali inavyokwenda kinachofanyika siyo kutengeneza Katiba Mpya, bali kufanya marekebisho makubwa katika katiba iliyopo,” alisema Arfi.

Jumapili, 24 Agosti 2014

UKAWA YAPATA PIGO

Dodoma.  
Bunge Maalumu la Katiba, jana liliridhia azimio la kuzifanyia marekebisho kanuni zake saba bila kuwapo kwa wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao wamesusia Bunge hilo.

Marekebisho hayo ya kanuni yanaonekana kuwa pigo kubwa kwa wajumbe hao wa Ukawa kwa vile sasa hawatapewa tena fursa ya kufafanua maoni ya wachache badala yake watasoma tu.
Awali, Kanuni ya 33 ilikuwa ikitaka mwenyekiti wa kamati kutumia muda wa dakika 60 kusoma taarifa yake iliyokuwa ikijumuisha maoni ya wajumbe walio wengi na taarifa ya wale walio wachache.
Lakini kanuni hiyo sasa imefanyiwa marekebisho, ambapo mwenyekiti wa kamati atasoma tu taarifa ya walio wengi na maoni ya walio wachache yatasomwa na mmoja wa wajumbe wa walio wachache.
Kanuni hiyo ya 33(5) sasa itasomeka: “Maoni ya wajumbe walio wachache yatasomwa na mmoja wa wajumbe ambao hawakuunga mkono maoni ya wajumbe walio wengi kwa muda usiozidi dakika 30.”
Akiwasilisha maelezo ya Kamati ya Maadili na Haki za Bunge, mjumbe wa kamati hiyo, Evod Mmanda, alisema kuwa hakutakuwa na nafasi tena ya mjumbe kutoka kundi la wachache kutoa mambo kichwani.
Mmanda aliyekuwa akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa kamati hiyo, Pandu Ameir Kificho, alisema maoni ya wachache yaligeuzwa kuwa maoni ya kisiasa na kubeba hoja za kishabiki za kisiasa. Alisema kuwa kutokana na marekebisho hayo, hakuna jambo litakalokuwa halijajadiliwa kwenye kamati, ambalo litaruhusiwa kusomwa na walio wachache ndani ya Bunge Maalumu la Katiba.
Kanuni nyingine zilizorekebishwa ni pamoja na ya 32, ambayo sasa inaruhusu mjumbe yeyote au kundi lolote la wajumbe kupendekeza sura mpya kwenye Rasimu ya Katiba.
Rasimu iliyowasilishwa bungeni na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ina Sura 17.
Kanuni nyingine zilizorekebishwa ni 35, 41, 60, 62 na 82 pamoja na sehemu inayohusu orodha ya yaliyomo katika kanuni hizo za Bunge za mwaka 2014.
Akichangia hoja ya marekebisho hayo, mjumbe wa Bunge hilo, Anjelina Samike alisema kwamba wajumbe kutoka kundi la walio wachache walikuwa na maneno magumu na yasiyo na staha.
Kwa upande wake, Yusuph Singo alisema nafasi waliyokuwa wakipewa walio wachache,  hawakuitumia kutoa ufafanuzi, badala yake waliitumia kujadili na kuibua mambo mapya.

Kituo cha Shirika la Utangazaji Tanzania Kanda ya kati Dodoma Kilizinuliwa rasmi mwaka 1988 na Waziri mkuu na makamu wa kwanza wa Rais Jaji Joseph S. Warioba.