Jumapili, 24 Agosti 2014

UKAWA YAPATA PIGO

Dodoma.  
Bunge Maalumu la Katiba, jana liliridhia azimio la kuzifanyia marekebisho kanuni zake saba bila kuwapo kwa wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao wamesusia Bunge hilo.

Marekebisho hayo ya kanuni yanaonekana kuwa pigo kubwa kwa wajumbe hao wa Ukawa kwa vile sasa hawatapewa tena fursa ya kufafanua maoni ya wachache badala yake watasoma tu.
Awali, Kanuni ya 33 ilikuwa ikitaka mwenyekiti wa kamati kutumia muda wa dakika 60 kusoma taarifa yake iliyokuwa ikijumuisha maoni ya wajumbe walio wengi na taarifa ya wale walio wachache.
Lakini kanuni hiyo sasa imefanyiwa marekebisho, ambapo mwenyekiti wa kamati atasoma tu taarifa ya walio wengi na maoni ya walio wachache yatasomwa na mmoja wa wajumbe wa walio wachache.
Kanuni hiyo ya 33(5) sasa itasomeka: “Maoni ya wajumbe walio wachache yatasomwa na mmoja wa wajumbe ambao hawakuunga mkono maoni ya wajumbe walio wengi kwa muda usiozidi dakika 30.”
Akiwasilisha maelezo ya Kamati ya Maadili na Haki za Bunge, mjumbe wa kamati hiyo, Evod Mmanda, alisema kuwa hakutakuwa na nafasi tena ya mjumbe kutoka kundi la wachache kutoa mambo kichwani.
Mmanda aliyekuwa akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa kamati hiyo, Pandu Ameir Kificho, alisema maoni ya wachache yaligeuzwa kuwa maoni ya kisiasa na kubeba hoja za kishabiki za kisiasa. Alisema kuwa kutokana na marekebisho hayo, hakuna jambo litakalokuwa halijajadiliwa kwenye kamati, ambalo litaruhusiwa kusomwa na walio wachache ndani ya Bunge Maalumu la Katiba.
Kanuni nyingine zilizorekebishwa ni pamoja na ya 32, ambayo sasa inaruhusu mjumbe yeyote au kundi lolote la wajumbe kupendekeza sura mpya kwenye Rasimu ya Katiba.
Rasimu iliyowasilishwa bungeni na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ina Sura 17.
Kanuni nyingine zilizorekebishwa ni 35, 41, 60, 62 na 82 pamoja na sehemu inayohusu orodha ya yaliyomo katika kanuni hizo za Bunge za mwaka 2014.
Akichangia hoja ya marekebisho hayo, mjumbe wa Bunge hilo, Anjelina Samike alisema kwamba wajumbe kutoka kundi la walio wachache walikuwa na maneno magumu na yasiyo na staha.
Kwa upande wake, Yusuph Singo alisema nafasi waliyokuwa wakipewa walio wachache,  hawakuitumia kutoa ufafanuzi, badala yake waliitumia kujadili na kuibua mambo mapya.

Kituo cha Shirika la Utangazaji Tanzania Kanda ya kati Dodoma Kilizinuliwa rasmi mwaka 1988 na Waziri mkuu na makamu wa kwanza wa Rais Jaji Joseph S. Warioba.